Home » Tanzania » Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 42 kuanzia sasa

Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 42 kuanzia sasa

20 December 2018 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly  tarehe 12 Desemba, 2018 wameshuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 42 kuanzia sasa.

Mkataba huo umetiwa saini kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka na wawakilishi wa kampuni za ujenzi kutoka Misri ambao ni Mwenyekiti wa kampuni ya Arab Contractors Bw. Mohamed Mohsen Salaheldin na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Bw. Ahmed Sadek Elsewedy.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Tanzania na Misri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, Wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo, Mhe. Rais Magufuli amesema ujenzi wa mradi huo utakaozalisha megawatts 2,115 za umeme utagharimu shilingi Trilioni 6.558, fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Tanzania na katika kipindi cha miaka zaidi ya 60 ya uhai wake mradi huu utaiwezesha Tanzania kupata umeme mwingi, wa uhakika na wa gharama nafuu kwa ajili ya matumizi ya majumbani na biashara ikiwemo viwanda.

“Kwa hivi sasa nchi yetu ina megawatts 1,560 tu za umeme, mradi huu pekee yake utazalisha megawatts 2,115. Uzuri ni kwamba umeme unaozalishwa kwa kutumia maji ni nafuu sana (shilingi 36/- tu kwa uniti moja) ikilinganishwa na umeme wa vyanzo vingine (mfano umeme wa mafuta unaofikia shilingi 446/- kwa uniti moja)” ametoa mfano Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa mengine kama vile kuimarisha uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya mradi, mifugo ikiwemo wanyamapori kupata maji ya kutosha, kilimo cha umwagiliaji, kuvutia utalii, uvuvi na kukuza ujenzi wa viwanda, tofauti na madai ya baadhi ya watu wanaodai kuwa utaharibu mazingira.

“Eneo lote la mradi huu ni sawa na asilimia 1.8 hadi 2 tu ya pori zima la hifadhi ya akiba ya Selous, kuwepo kwa mradi huu kutasaidia watu wengi kupika kwa kutumia umeme badala ya kuni na mkaa ambao takwimu zinaonesha umekuwa ukisababisha kukatwa kwa hekta 583 za miti kila siku. Tuna imani kubwa ukikamilika wananchi wengi wataachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia umeme utakaopatikana kwa bei nafuu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuunga mkono juhudi za Serikali kutekeleza mradi huu na amewataka wanaotumiwa na mabeberu kupiga juhudi hizi waache kwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote bila kubagua itikadi ya siasa, dini ama kabila la mtu.

Pia amewashukuru viongozi wa Dini waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo na kuomba dua njema kwa mradi na Taifa, pamoja na viongozi wengine wote kwa kutambua umuhimu wa mradi huu mkubwa.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly kwa ujio wake hapa nchini na amemuomba amfikishie salama za shukrani kwa Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah el-Sisi kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Misri na ameahidi kuuendeleza na kuukuza uhusiano huu.

Waziri Mkuu wa Misri Mhe. Dkt. Mustafa Madbouly amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri wa Tanzania na Misri ulioasisiwa na viongozi wa Mataifa haya Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Gamal Abdel Nasser, na ameahidi kuwa pamoja na kutekeleza mradi huu Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine ya biashara na uwekezaji pamoja na kuunga mkono juhudi mbalimbali za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Nao viongozi mbalimbali waliopata fursa ya kutoa salamu katika tukio hilo wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa anazozifanya katika uongozi wake ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuhakikisha nchi ina amani, kulinda hadhi ya nchi na kuhakikisha nchi inajenga misingi ya kujitegemea na wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa manufaa ya Taifa.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

12 Desemba, 2018

Ad