Home » Tanzania » Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu

27 November 2016 | Tanzania

 

Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu leo tarehe 27 Novemba, 2016 majira ya jioni amewasili hapa nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku 3 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Lungu amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini pamoja na wananchi.

Akiwa uwanjani hapo Rais Lungu amepokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kesho tarehe 28 Novemba, 2016 Rais Lungu ataendelea na ziara yake hapa nchini ambapo pamoja na kutembelea miradi ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo TAZARA na TAZAMA, atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, atashuhudia utiaji saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia na jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais Magufuli kwa ajili yake Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Chad Mhe. Idriss Deby Itno leo tarehe 27 Novemba, 2016 majira ya alasiri amewasili hapa nchini kwa ziara kikazi ya siku 2.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Rais Idriss Deby Itno akiwa na Mkewe Mama Hinda Deby amepokelewa na mwenyeji wake Rais Magufuli na kisha kulakiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na wananchi.

Jioni hii, Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Rais Idriss Deby Itno Ikulu Jijini Dar es Salaam.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

27 Novemba, 2016

Ad