Home » Tanzania » Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation)

Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation)

13 February 2018 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) na Bw. Waziri Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.

Uteuzi wa Dkt. Omari Rashid Nundu na Bw. Waziri Waziri Kindamba umeanza tarehe 01 Februari, 2018.

Kabla ya Uteuzi huu Dkt. Omari Rashid Nundu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (Tanzania Telecommunication Company Limited – TTCL) na Bw. Waziri Waziri Kindamba alikuwa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo.

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ilibadilishwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2017 na kuwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutia saini sheria namba 12 ya mwaka 2017 ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) na tarehe 01 Februari, 2018 TTCL Corporation ilianza kufanya kazi rasmi.

Pamoja na kufanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwahamisha wafanyakazi wote na maafisa wa umma (Employees and Public Officers) wa iliyokuwa TTCL kwenda TTCL Corporation.

Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa kutoivunja bodi ya iliyokuwa TTCL, wajumbe wake wote kuendelea na nafasi zao na kujaza nafasi za wajumbe zilizobaki ikiwa ni pamoja na nafasi moja ya mjumbe kutoka Zanzibar.

 

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

12 Februari, 2018

Ad