Home » Tanzania » Rais Magufuli aweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja jipya la Selander Jijini Dar es Salaam

Rais Magufuli aweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja jipya la Selander Jijini Dar es Salaam

20 December 2018 | Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Desemba, 2018 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja jipya la Selander linalounganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Daraja hilo lenye urefu wa meta 1,030 na upana  wa meta 20.5 litakuwa na njia 4 za magari na njia 2 za watembea kwa miguu, na litajengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.

Sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika katika eneo la Aga Khan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Makonda.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja hilo utakaochukua muda wa miezi 30 kuanzia tarehe 23 Julai, 2018 utagharimu shilingi Bilioni 256 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.

Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa daraja hilo litadumu kwa muda wa miaka 100 na litajengwa bila kuathiri nyumba zilizopo kando ya barabara za Kenyatta na Toure ambazo miongoni mwake wanaishi Mabalozi.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kufadhili ujenzi wa daraja hilo na amemuomba Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Cho Tae-ick kufikisha ujumbe wake kwa Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Moon Jae-in kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hiyo hususani wakati huu ambapo inaendelea kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

“Jamhuri ya Korea ni marafiki wetu wa kweli, wametusaidia kujenga daraja la Kikwete katika mto Malagarasi na wametusaidia kujenga Hospitali ya Taaluma na Sayansi ya Tiba Mloganzila na miradi mingine, tunawashukuru sana, naomba na sisi Watanzania tubadilike, tuchape kazi, tuwe wazalendo, tuwahimize vijana wetu waje wafanye kazi kwenye mradi huu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta jina la daraja jipya la Selander na amependekeza lipewe jina la Tanzanite linaloakisi Utanzania.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wote kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa huku wakitanguliza uzalendo, kudumisha amani na upendo na kutokukatishana tamaa ili Tanzania ifanikiwe kupiga hatua za kimaendeleo kama ilivyofanya Jamhuri ya Korea ambayo uchumi wake ulikuwa sawa na Tanzania miaka ya 60 wakati Tanzania ikipata uhuru.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kwa juhudi zake za kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwemo kuhakikisha mabasi yote 49,000 yaliyopo nchini yanaanza kutoa tiketi za kielekroniki, kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya usafirishaji kwa njia ya reli na kufuatilia meli moja kubwa iliyonunuliwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China ili ianze kuja nchini na kuinufaisha Tanzania.

Mapema katika salamu zake Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea Mhe. Cho Tae-ick ameishukuru Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea ambapo katika kipindi cha miaka 26 ya uhusiano huo, Jamhuri ya Korea imetoa ufadhili wenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 1 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa ufadhili wa nchi hiyo Barani Afrika.

Nae mwakilishi wa EDCF Mhe. Hyon-jong Lee amesema kwa umuhimu wa kipekee wa uhusiano ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, Serikali za nchi hizo zinaendelea na majadiliano ya ufadhili wa miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 687.6 itakayotekelezwa nchini Tanzania katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.

 

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

20 Desemba, 2018

Ad