Home » Tanzania » Raia wa Kigeni 15 katika mgodi wa Tanzanite One wafukuzwa nchini.

Raia wa Kigeni 15 katika mgodi wa Tanzanite One wafukuzwa nchini.

14 January 2016 | Tanzania
Jumla ya raia wa kigeni 15 waliobanika kufanya kazi kinyume na taratibu za kisheria  katika mgodi wa Tanzanite One uliopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wameondoshwa nchini tarehe 25 Desemba, mwaka jana.
 
Hayo yalielezwa jana jijini Arusha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, Amos Makala wakati wa kikao chake na wajumbe wa kamati  hizo pamoja na Naibu Katika Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe kilichofanyika katika Kituo cha  Jimolojia jijini humo.
 
Alisema kuwa raia hao waliamuliwa kuondoka nchini na Idara ya Uhamiaji mkoani Manyara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo ambazo ziliunda kikosi kazi cha wajumbe 13 kwa ajili ya udhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi, ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni zinazoshughulika na biashara ya madini na kuchunguza raia wa kigeni wasiokuwa na sifa za kufanya kazi kwenye migodi pamoja na kampuni za madini. 
 
 “Amri hiyo ya kuondoka nchini ndani ya siku saba ilianza kutekelezwa kuanzia tarehe 17 Desemba, 2015 na raia wote hao waliofukuzwa  wanatoka nchini India. Nakipongeza Kikosi kazi hiki ambacho kimeanza kutekeleza majukumu ya kamati kwa ufanisi na zoezi hili litakuwa ni endelevu,” alisema Makala. 
 
Aidha, alisema kuwa kikosi kazi hicho kilifanya operesheni ya siku mbili katika Mikoa hiyo kwa lengo la kukamata wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite ambao hawana leseni ambapo  jumla ya wafanyabiashara 15 walikamatwa mkoani Arusha wakati mkoani Manyara idadi ya wafanyabiashara waliokamatwa kwa tuhuma za aina hiyo ni Nane na madini waliyokamatwa nayo yana thamani ya takribani shilingi milioni 47.  
 
Alisema kuwa operesheni hiyo iliyofanyika tarehe 30 na 31 mwezi Desemba mwaka jana ilijikita pia katika kuwabaini raia wa kigeni wanaofanya biashara ya madini bila vibali ambapo raia mmoja kutoka nchini Ethiopia alikamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara ya madini kinyume na sheria na anatarajiwa kufikishwa Mahakamani mara baada ya taratibu za awali za kipelelezi kukamilika.
 
Awali, Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho, Muliro Muliro ambaye pia ni Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha alisema kuwa baada ya zoezi la kuwabaini pamoja na kuwakamata wafanyabiashara wa madini wasiokuwa na vibali, jumla ya wafanyabiashara 272 ambao walikuwa wakifanya biashara hiyo kinyemela walijitokeza katika Ofisi za Madini za Arusha na Merelani ili kuomba leseni za kufanya biashara hiyo.
 
“Mkoani Manyara (Merelani) ilipo migodi ya Tanzanite jumla ya wafanyabiashara 154 walijitokeza na kuwasilisha maombi ya leseni za wakala wa madini ya vito (brokers’ licence) na hivyo hadi kufikia tarehe 8 Januari mwaka huu, kiasi cha shilingi milioni 38.5 zilikusanywa kutokana na ada ya maombi ya leseni husika,” alisema Muliro.
 
Vilevile alisema kuwa kwa upande wa Arusha, maombi mapya ya leseni za wakala wa madini yapatayo 115 yaliwasilishwa Ofisi za Madini za kanda ya Kaskazini na hivyo kiasi cha shilingi milioni 28.7 kimekusanywa kutokana na maombi hayo.
 
Naye Naibu Katibu Mkuu, Profesa Mdoe alizipongeza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo kwa kazi nzuri wanayofanya kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini katika kudhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi, kubaini wafanyabiashara wa madini hayo wasiokuwa na vibali na wanaokwepa kulipa kodi stahiki.
 
Alisema kuwa bado kuna kazi kubwa mbele ya kuhakikisha kuwa suala hilo linakomeshwa na kusisitiza kwamba kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo huku akieleza kuwa operesheni haitoweza kumaliza tatizo hilo kama watumishi hawatatimiza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi ili kutotoa mianya kwa matatizo hayo kuendelea kuwepo.
Ad