Home » Tanzania » MV Nyerere: Rais Magufuli asema dereva aliyepaswa kuendesha MV Nyerere hakuwepo

MV Nyerere: Rais Magufuli asema dereva aliyepaswa kuendesha MV Nyerere hakuwepo

23 September 2018 | Tanzania

Sasa imebainika kwamba nahodha wa kivuko cha MV Nyerere kilichozama Alhamisi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 hakuwepo katika feri hiyo wakati ilipozama.

Akihutubia taifa siku ya Ijumaa jioni rais wa Jamhuri ya Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa ana habari kwamba nahodha huyo alimwachia zamu ya kuendesha chombo hicho mtu ambaye hakuwa amepata mafunzo ya kazi hiyo.

Akizungumza moja kwa moja kupitia runinga, rais Magufuli amesema kuwa nahodha huyo tayari amekamatwa na polisi .

Aidha rais Magufuli ameagiza wale wote wanaohusika na operesheni za kivuko hicho kukamatwa ili kuhojiwa.

Kulingana na Magufuli huenda sababu ya kuzama kwa chombo hicho ni 'kujaa kupitia kiasi'.

Lakini amesema kuwa kamati itakayoundwa itasaidia kutoa maelezo zaidi.

Takriban miili 211 imeopolewa kufikia sasa , kulingana na idadi ya mwisho iliotolewa kabla ya rais Magufuli kutoa hotuba yake.

Magufuli alisema: Ni wazi kwamba miili zaidi imekwama ndani ya chombo hicho, Ripoti nilizopoikea zinaonyesha kuwa hata mizigo iliobebwa ilikuwa zaidi ya kiwango cha tani 25 zinazoruhusiwa.

Kulikuwa na tani za mahindi, kreti za pombe, vifaa vya umeme na Ujenzi. Abiria pia walikuwa wamebeba mizigo mikubwa kwa kuwa walikuwa wanatoka katika soko.

Kiongozi huyo ametangaza siku nne za kuomboleza kutoka siku ya Ijumaa huku bendera ya taifa hilo ikipepea nusu mlingoti.

Aidha amewaonya baadhi ya wanasiasa dhidi ya kuchukua fursa ya mkasa huo ili kujipatia umaaarufu wa kisiasa.

''Tuwache mamlaka ifanye kazi yake na iwapo una ushahidi unahitaji kusubiri hadi wakati swala hilo litawasilishwa mahakamani ili kuweza kuisadia mahakama kutoa haki''

Ad