Home » Tanzania » Makamu wa Rais afungua maonyesho ya Kibiashara kati ya Ufaranza na Tanzania yanayofanyika Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais afungua maonyesho ya Kibiashara kati ya Ufaranza na Tanzania yanayofanyika Jijini Dar es Salaam

04 April 2017 | Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Tanzania ni Moja ya nchi salama kwa ajili ya uwekezaji barani Afrika kwa sababu haina matatizo ya migogoro ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa mali ya wawekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akifungua maonyesho ya Kibiashara kati ya Ufaranza na Tanzania yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.

Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hasa katika kilimo, nishati, utalii,usafiri kutokana na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini.

Makamu wa Rais amesema maonyesho hayo ya kibiashara ambayo yataambatana na kongamano kubwa la Kibiashara kati ya nchi hizo Mbili ni fursa ya kipekee kwa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa kukutana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji.

Ameeleza kuwa katika kuelekea katika uchumi wa viwanda Tanzania haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake bali kwa kushirikiana na mataifa makubwa ambayo yamekuwa na teknolojia ya kisasa katika uwekezaji ikiwemo taifa la Ufaransa.

Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza nchini kuwa serikali itafanya kila linalowekezekana kuendelea kujenga mazingira bora kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo bandari, reli, barabara, usafiri wa anga ili kurahisisha kazi ya usafiri na usafirishaji nchini.

Kwa upande wake, Balozi Ufaransa hapa nchini Malika Berak amesema kuwa ufunguzi wa Kongamano hilo kubwa la Kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa linalolenga kujenga na Kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo Mbili.

Balozi huyo amesema kuwa kongamano hilo litajikita katika kujadili kwa kina fursa za uwekezaji hapa nchini hasa kwenye maeneo ya nishati, usafirishaji, teknolojia ya habari na Mawasiliano na miradi ya maendeleo.

Kongamano hilo la siku NNE la Kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania litawakutanisha wafanyabiashara wa Kitanzania na wenzao wa Ufaransa katika kujadili na kubadilisha uzoefu katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kibiashara kama hatua ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

Ikulu- Dar es Salaam.

4-Apr-2017.

Ad