Home » Nje Ya Afrika » Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu wa Japan

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu wa Japan

19 April 2016 | Nje ya Afrika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe kufuatia vifo vya watu zaidi ya 40 vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi lililokikumba kisiwa cha Kyushu kilichopo kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Tetemeko hilo la ardhi limetokea Alhamisi iliyopita tarehe 14 Aprili, 2016 na kurudia tena siku ya Jumamosi tarehe 16 Aprili, 2016 ambapo limesababisha maporomoko makubwa ya udongo yaliyoharibu na kufunika makazi ya watu na miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano.

Katika salamu hizo zilizopitia kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo mbaya na amempa pole nyingi Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe.

"Nakupa pole sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Shinzo Abe, na kupitia kwako natoa pole kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo" Amesema Rais Magufuli.

Aidha, Dkt. Magufuli amewapa pole wote waliojeruhiwa wakati wa maporomoko ya udongo, na amewaombea wapone haraka ili waweze kuungana na wananchi wengine wa Japan katika shughuli za kila siku za ujenzi wa Taifa lao.

Pia amevitakia kila la heri vikosi vya uokoaji vinavyoendelea na kazi hiyo katika maeneo yote yaliyoathirika.

 

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

19 Aprili, 2016

 

Ad