Home » Michezo » CHAN 2016: Rwanda yatinga robo fainali

CHAN 2016: Rwanda yatinga robo fainali

21 January 2016 | Michezo

Timu ya taifa ya soka ya Rwanda, imekuwa nchi ya kwanza kufuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano ya soka baina ya wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani CHAN.

Amavubi Stars imefuzu baada ya kuishinda Gabon mabao 2 kwa 1 katika mchuano wake wa pili siku ya Jumatano jioni hii katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.

Hadi sasa, Rwanda inaongoza kundi la A kwa alama sita baada ya kupata ushindi katika mchuano wake wa kwanza Jumamosi iliyopita, walipoifunga Cote Dvoire bao 1 kwa 0 na watamenyana katika hatua ya robo fainali na mshindi wa pili wa kundi B.

Ivory Coast nao wamejiweka katika nafasi nzuri baada ya kuifunga Morroco bao 1 kwa 0 katika mchuano wake wa pili, pia uliochezwa jana katika uwanja wa Amahoro.

Tembo hao kutoka Afrika Magharibi, wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 3 na mchuano wao wa mwisho utakuwa dhidi ya Gabon siku ya Jumapili katika uwanja wa Huye.

Ivory Coast wanahitaji sare, au ushindi kusonga mbele na kuomha kuwa Morocco wanawashinda Rwanda katika mchuano wake wa mwisho utakaochezwa pia Jumapili katika uwanja wa Amahoro.

Gabon pia wanaweza kufuzu ikiwa wataifunga Ivory Coast na Rwanda kuishinda Morocco.

Siku ya Alhamisi, mechi za kundi B zinaendelea.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itachuana na Angola katika uwanja wa Huye mjini Butare kuanzia saa kumi jioni, na baadaye Cameroon watamenyana na Ethiopia.

 

 

Ad