Home » Biashara » Wachuuzi wa Tanzaniate wazungumzia leseni

Wachuuzi wa Tanzaniate wazungumzia leseni

15 January 2016 | Biashara
Na Woinde Shizza.
WACHUUZI wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kutowabana walipe leseni ya ununuzi, kwani uwezo wao ni mdogo na wao ni madalali siyo wanunuzi wa madini hayo.
Wakizungumza juzi wachuuzi hao walidai kuwa hawapingi kulipa mapato ya serikali ila zoezi la ulipaji wa leseni ya kununulia madini ya Tanzanite ingetakiwa kutekelezwa kwa wafanyabiashara peke yao na siyo kwa wachuuzi wadogo.
Mmoja kati ya wachuuzi hao Anturusia Chande alisema wengi wao wanapewa madini hayo na kuzunguka kwenye masoko ya Mirerani kwa lengo la kujikimu maisha yao ikiwemo kusomesha watoto, mavazi, chakula na matibabu. 
“Sisi hatuvuki na madini nje ya eneo la Mirerani na tunategemea kuendesha maisha yetu kupitia uchuuzi huu mdogo mdogo na pia hatuna mtaji kwani tumejiajiri wenyewe serikali ituangalie kwa kupitia hili,” alisema Chande.
 
Alisema wao wanachangia pato la Taifa kupitia sekta hiyo kwa kulipa kodi pindi wanaponunua bidhaa mbalimbali madukani ikiwemo sukari, mchele, mafuta ya kula, ya taa, sigara na nyinginezo ila bado wanasumbuliwa na serikali. 
Kaanael Minja alisema zoezi la kuwakamata wachuuzi ambao hawakulipa leseni lililoendeshwa wiki iliyopita, halikufanyika kwa haki kwani kuna baadhi yao waliporwa madini ambayo siyo yao na hawakurudishiwa hadi hivi sasa. 
“Kabla ya kuendesha kamata kamata hiyo wangetoa elimu kwanza kwa wachuuzi hao lakini kitendo cha kufika kijiweni na kuanza kuwakamata watu wasio na leseni siyo kizuri, wangepaswa kuwaelimisha kwanza,” alisema Minja. 
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mahmoud Kambona aliwataka wachuuzi hao kujipanga na kulipia leseni ya ununuzi wa madini hayo ili waongeze mapato kwa serikali ambayo inawaletea wananchi maendeleo.
“Wanatakiwa kutambua kuwa hiyo ni sheria ambayo imepitishwa na sasa kinachotakiwa ni utekelezaji kwani serikali zote hujiendesha kutokana na kodi ambazo zinalipwa na wananchi wake na siyo vinginevyo,” alisema Kambona.
Ad