Home » Biashara » Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo kwa Uongozi wa Baraza la Mji wa Wete

Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo kwa Uongozi wa Baraza la Mji wa Wete

13 January 2016 | Biashara

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo
kwa Uongozi wa Baraza la Mji wa Wete Kisiwani Pemba kutoongeza wafanya
biashara wapya hadi wale wazamani wote watakapopatiwa nafasi za
kufanya biashara mara baada ya kumalizika kwa ujenzi wa soko jipya la
Mji huo.
Alisema wapo watendaji ndani ya Taasisi za umma waliozoea kutumia
madaraka yao kwa kuuza nafasi za biashara kwa wafanyabiashara wapya
wenye uwezo mkubwa na kuwaacha wale wa asili kwa sababu tu ya
kupenyezewa kitu kidogo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo mara baada ya kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa Soko Kuu la Matunda na Ofisi ya Baraza la Mji wa
Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za
maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Januri  1964
kutimia miaka 52 sasa.
Alisema Serikali iliyopo ni ya wengi wa wananchi wanyonge, hivyo kamwe
haitokubali kumvumilia mtendaji ye yote  asiyezingatia sheria na agizo
hilo na kuamua kutumia wadhifa wake kwa kuwanyanyasa wafanyabiashara
wa kipato cha chini.
Alieleza kwamba Taifa limekusudia kuwa na masoko makubwa ya kisasa
katika Miji yote ya Unguja na Pemba ili kusaidia kupunguza tatizo la
ajira kwa wananchi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora katika
masoko hayo.
“ Kumalizika kwa ujenzi wa soko la Wete kutaongeza nafasi za kufanyia
biashara kama vile maduka, nafasi za kuuzia mboga mboga na matunda
mambo ambayo yatapelekea kutoa nafasi kwa wananchi walio wengi
kujiajiri wenyewe “. Alisema Balozi Seif.
Alisema hatua hiyo ya Serikali pia italiwezesha Baraza la Mji wa Wete
kukusanya mapato mengi kutokana na ongezeko  kubwa la wafanyabiashara
kasi ambayo italipa nguvu za ziada kutoka huduma bora kwa wakaazi wake
pamoja na wageni watakaohitaji huduma za kibiashara katika eneo hilo.
Mkamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Benki ya Wananchi
wa Zanzibar { PBZ } kufikiria kuweka huduma zao mara utakapokamilika
ujenzi wa soko hilo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za fedha
kwa urahisi.
“ Soko hili la Wete litakapokamilika ujenzi wake litakuwa miongoni mwa
masoko ya kisasa lenya wafanyabiashara wengi zaidi ambao watafanya
kazi katika mazingira bora “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato ambalo Masoko ni miongoni
mwa vianzio vikubwa vya mapato vya Mabaraza ya Miji na Halmashauri za
Wilaya, Ballozi Seif alishauri wakati umefika kwa watendaji wa taasisi
hizo kuanzisha mfumo wa kisasa wa ukusanyaji mapato kwa kutumia
mtandao wa Kompyuta.
 Alisema mfumo huu wa kisasa  unaotumia mashine za Kisasa za
kielektoniki umeonekana kuleta mafanikio ya haraka na kuachana na ule
zamani wa kukusanya mapato kwa kupitia vibanda na risiti mkononi ukiwa
ukepitwa na wakati.
Alifahamisha kwamba ukusanyaji  wa mapato unaotumika hivi sasa katika
masoko mbali mbali nchini bado unaendelea kutoa mwanya kwa mapato
mengi kuingia kwenye mifuko ya wajanja.
Akigusia suala la usafi wa mazingira katika masoko ya mabaraza ya Miji
na Halmashauri za Wilaya Balozi Seif alipendekeza kuanzishwa kwa
utaratibu maalum wa kusafisha masoko hayo.
Alisema si vibaya kwa Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum
za SMZ kuanzisha mashindano ya usafi wa masoko kila mwaka na mshindi
kusawadiwa zawadi nono inayostahiki.
Balozi Seif alieleza kwamba utaratibu huo unaweza kusaidia sana Masoko
hayo katika utunzaji wa mazingira katika kiwango kinachokubalika jambo
ambalo pia litatoa fursa kwa wafanyabiashara wanaotumia muda wao
mkubwa sehemu hizo kuishi katika mazingira rafiki.
“ Masoko mengi yanapokuwa mapya hufuata taratibu zote za utunzaji wa
usafi wa  mazingira lakini hali hiyo hatimae hupotea baada ya kipindi
kifupi na watu kusahau kwamba uzorotaji wa usafi katika maeneo hayo
huhatarisha maisha ya Wananchi “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Benkiu ya Dunia { WB }
kwa kukubali kugharamia ujenzi wa soko la Mji wa Wete na kuiomba
Kampuni iliyopewa kazi za ujenzi huo kuhakikisha inakamilisha mradi
huo kwa wakati ili Wananchi wanufaike nahuduma bora zinazotarajiwa
kupatikana katika soko hilo.
Akisoma risala Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Nd. Mgeni Othman
alisema ujenzi wa soko la Mji wa Wete ulioanza Tarehe 4 Aprili mwaka
2015 na kukamilika rasmi tarehe 3 April mwaka huu unatarajiwa
kuwafaidisha wakaazi 31,872 wa shehia 8 zilizouzunguuka Mji huo.
Nd. Othman alisema soko kuu la Matunda Mjini Wete litakuwa na milango
35 ya Biashara, Vikuta 80 vya uuzaji wa matunda, Banda la abiri, Ofisi
15 za wafanyakazi wa baraza la Mji,kituo cha Dala dala pamoja na vyoo.
Mkurugenzi huyo wa Baraza la Mji wa Wete alieleza kwamba zipo
changamoto zilizojitokeza ndani ya ujenzi wa majengo ya soko hilo
zilizopelekea kushindwa kujengwa kwa jingo la biashara ya uuzaji wa
kuku kutokana na sehemu ya eneo hilo kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba
mbili za makaazi ya watu.
Nd. Othman aliitaja changamoto nyengine iliyochangia ufinyu wa eneo la
Barala la Mji wa Wete ni  kituo cha mafuta  ambacho hakimo ndani ya
umiliki wa Baraza hilo la Mji wa Wete.
Akitoa Taarifa ya ujenzi wa Soko Kuu la Matunda la Mji wa Wete Katibu
Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum
Zanzibar Nd. Joseph Meza alisema Miji ya Bopwe, Limbani pamoja na
Kizimbani hivi sasa inahitaji kuwa na masoko yake.
Nd. Meza alisema hali hiyo kwa sasa inatokana na kukuwa na Mitaa ndani
ya Mji wa Wete pamoja na ongezeko la watu linalohitaji huduma hizo
muhimu kwa maisha ya kila siku ya wanaadamu.
Ujenzi wa Soko Kuu la Matunda na Ofisi ya Baraza la Mji wa Wete Mkoa
wa Kaskazini Pemba unafanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya Mkandarasi wa Kampuni ya Small Investment of Town Council {
STC } kwa mkopo wa shilingi Bilioni 1,597,383,432.40/- zilizotolewa na
Benki ya Dunia { WB }.

 

Ad