Home » Benki Kuu » Serekali ya awamu ya tano yavunja rekodi kusanyaji wa mapato

Serekali ya awamu ya tano yavunja rekodi kusanyaji wa mapato

15 January 2016 | Benki Kuu

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SERIKALI YA AWAMU YA TANO YAVUNJA REKODI KATIKA UKUSANYAJI MAPATO

Serikali ya awamu ya Tano imevunja rekodi katika ukusanyaji wa mapato kwa mwezi Desemba mwaka 2015 kwa asilimia 18.9 zaidi ya lengo lililokusudiwa. Serikali ilikuwa na maoteo ya kukusanya Sh. Trilioni 1 na bilioni 338 lakini makusanyo halisi yaliyopatikana ni Sh. Trilioni 1 na bilioni 592.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango, alisema kuwa maoteo ya mapato ya kodi kwa mwezi Desemba yalikuwa Sh.Trilioni 1 na bilioni 260 lakini makusanyo yaliyopatikana yalifikia Sh. Trilioni 1 na bilioni 403 hivyo kuvuka lengo kwa asilimia 11.5. “Kwa upande wa mapato yasiyo ya kodi maoteo yalikuwa Sh. Trilioni 0.077 na makusanyo halisi yalikuwa Sh. Trilioni 0.0183 sawa na asilimia 145.5 rekodi ambayo haijawahi kufikiwa toka Tanzania ipate uhuru”, alisisitiza Dkt. Mpango. Aidha, Dkt. Mpango alifafanua kuwa Serikali ikiendeleza jitihada hizi Tanzania itaondokana na utegemezi.

“Nawashukuru watanzania waliolipa kodi stahiki, waliozoea kukwepa kodi waache ili Serikali iweze kutoa huduma kwa wananchi,”Aliongeza. Ukusanyaji huo mkubwa wa mapato, umeiwezesha Serikali ya awamu ya tano kutekeleza ahadi yake ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari nchini. Akiendelea kutoa ufafanuzi Dkt. Mpango alisema kuwa mpaka sasa Hazina imeshapeleka kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri zote nchini, na kubainisha kuwa katika fedha hizo bilioni 15.7 zimepelekwa katika akaunti za shule na bilioni 3 zimepelekwa katika vyombo vya kusimamia mitihani.

Kufuatia utekelezaji huo Dkt. Mpango amewataka wakuu wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha hizo na kutoa wito kwa wakuu wa shule kuweka katika mbao za matangazo taarifa zote za fedha hizo ili kutoa fursa kwa wananchi kupata taarifa sahihi za matumizi. “Yeyote atakayetumia Fedha hizo tofauti na matumizi yaliyopangwa, Serikali itamchukulia hatua kali, na ninatoa wito kwa wananchi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa watakapoona fedha hizo zimetumika vinginevyo”.

Alisisitiza Dkt. Mpango. Naye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu ameeleza kuwa nchi ipo kwenye jitihada za kuhakikisha inapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza uuzaji wa bidhaa za ndani nje ya nchi ili kuongeza thamani ya shilingi. Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango alitoa wito kwa kila Mtanzania kuwa mzalendo na kutimiza wajibu wake kwa kulipa kodi stahiki ili kufikia mwaka 2025 nchi iweze kufanikisha lengo la kufikia kipato cha uchumi wa kati. Imetolewa na Msemaji wa Wizara Wizara ya Fedha na Mipango 07 Januari, 2016