Home » Afrika » Kiongozi wa waasi Riek Machar hakufika jijini Juba siku ya Jumatatu kama ilivyotarajiwa.

Kiongozi wa waasi Riek Machar hakufika jijini Juba siku ya Jumatatu kama ilivyotarajiwa.

20 April 2016 | Afrika

Waangalizi wa utekelezwaji wa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini wanaonya kuwa kutorejea kwa kiongozi wa waasi Riek Machar jijini Juba siku ya Jumatatu au jana kama ilivyotarajiwa, kunahatarisha kuzua tena kwa mapigano nchini humo.

Mwenyekiti wa Waangalizi hao ambaye ni rais wa zamani wa Boswtana Festus Mogae anasema, ikiwa Machar hatafika Juba hivi karibuni kuna uwezekano mkubwa wa kuanza tena kwa mapigano nchini humo na kuvunjika kabisa kwa mkataba wa uundwaji wa serikali ya pamoja, serikali ambayo Riek Machar atakuwa Makamu wa kwanza wa rais.

Wasiwasi huu pia umeoneshwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa hatua ya kutowasili kwa Machar huku Marekani ikimshutumu kiongozi huyo wa waasi kwa kutokuwa na nia ya dhati ya kutekeleza mkataba huo uliofikiwa mwaka jana.

Lakini swali kubwa ni kwanini Machar hajarejea ? Serikali ya Juba na waasi wanalaumiana kwa kutowasili Machar.

Waasi wanasema, serikali ya Juba imekataa kiongozi wao awasili na wanajeshi zaidi jijini Juba pamoja na silaha nzitonzito tuhma ambazo Riek Machar akizungumza na kituo cha Al Jazeera amekanusha.

Serikali ya rais Kiir inasema wanajeshi wa waasi ambao tayari wako Juba ni 1,370 idadi ambayo serikali inasema inatosha na hivyo hakuna haja ya kuwasili kwa mamia ya wapiganaji wengine wa waasi.

Machar anasema mkataba wa amani unamruhusu kuja na wanajeshi 2,910 na yeye anataka tu kuandalama na wanajeshi 260 na anasisitiza kuwa yuko tayari kufika Juba.

Kwa hali hii, hatujui tumwamini nani kati ya serikali ya Juba na waasi.

Ad